WANANCHI WATAKIWA KUZINGATIA MATUMIZI SAHIHI YA DAWA
Posted on: September 24th, 2025Wananchi mkoani Kigoma washauriwa kuepuka matumizi ya dawa kiholela ili kuepuka madhara, akizungumza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni –Kigoma Kaimu Mkuu wa idara ya famasi Boniface Oledrimen amesema kuwa kutumia dawa bila kuzingatia maelekezo ya mtaalamu wa dawa inaweza kuleta athari hasi kwa mtumiaji na kushauri wananchi kuacha matumizi hayo ya holela.
“Leo tuko hapa lengo ni kuhakikisha wananchi wanaofika hospitalini kwetu wanakua na uelewa juu ya matumizi sahihi ya dawa, hivyo tuwaombe sasa kuachana na matumizi ya dawa bila maelekezo kutoka kwa wataalamu kwa sababu unapokosea matumizi inaweza kukuletea athari hasi kati mwili na jamii, ndiyo maana mara zote tumekua tukisisitiza kuuliza pale ambapo unakua haujaelewa maelekezo yam toa huduma wa dawa ili kujihakikishia usalama wa afya yako na uweze kupata matokeo tarajiwa Katiba matibabu yako” amesema Boniface Oledrimen.
Hata hivyo Meneja wa duka la dawa la Hospitali Mwita Wambura ameeleza kuwa wapo kinamama ambao huwapatia watoto dawa ambazo zimekwisha muda wake wa matumizi na kusema kuwa dawa nyingi za watoto aina ya syrup hutumika kwa siku saba na kisha zinatakiwa kutotumika tena lakini mara nyingi wananchi huendelea kuzitumia, hivyo zinaweza kuleta athari hasi kwa watoto.
“Kuna dawa hasa za watoto ambazo zinatakiwa kutumika ndani ya siku saba lakini kinamama wanatumia dawa hizo licha ya muda wake wa matumizi kuisha jambo ambalo siyo sahihi, hivyo dawa inapokuwa imeelekezwa kutumika ndani ya muda Fulani basi tuzingatie ili isiweze kuleta madhara kwa watoto” amesema Wambura.
Pia Nasra Payema ambaye ni mfamasia amesema licha ya kutofuata muda wa matumizi lakini wananchi wengi wamekuwa na utaratibu wa kutomaliza dozi ya dawa wanazopewa jamba ambalo amebainisha kuwa linaweza kuleta madhara huku akisema majawapo ni usugu wa vimelea dhidi ya dawa ambapo inaweza kusababisha kutokupona kwa wakati hivyo amewashauri wananchi kuacha matumizi holela ya dawa hasa dawa aina ya antibiotics, Pia alisisitiza juu ya umuhimu wa kumaliza dozi kamili kwa siku zote unazotumia dawa.
Kwa upande wake Joseph Hagai ambaye ni moja ya wananchi waliokua wakipata elimu hiyo katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma amesema ni vema elimu hii itolewe mara kwa mara, huku akiweka wazi kuwa wananchi wengi hawana elimu ya matumizi sahihi ya dawa.
“Kwanza mimi naweza nikasema nashukuru sana kwa kutupatia elimu hii, lakini ni watu wengi sana hawajui kuhusu haya mimi naona ni vema sasa elimu hii itolewe kwa watu mara kwa mara ili tuweze kuondokana na matatizo mbalimbali yanayotokana na matumizi ya daya yasiyo sahihi” Amesema Hagai.