MAWENI RRH KUSHIRIKIANA NA MUHAS NYANJA MBALIMBALI IKIWEMO TAFITI
Posted on: April 22nd, 2026
Chuo kikuu cha Muhimbili (MUHAS) kuanzisha ushirikiano na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma katika Nyanja mbalimbali ikiwemo utafiti, mafunzo na huduma, hayo yamebainishwa na Profesa. Emmanuel Ballandya, Makamu Mkuu wa Chuo – taaluma kupitia kikao kazi kilichowakutanisha viongozi mbalimbali wa Chuo hicho pamoja na uongozi wa Hospitali na kutembelea maeneo ya utoaji wa huduma leo tarehe 22 Aprili, 2026.
Akizungumza katika kikao hicho baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya kutolea huduma Profesa. Ballandya amesema tayari yapo mazingira bora ya utoaji wa huduma ambayo yatasaidia katika kufanya tafiti mbalimbali pamoja na kutoa nafasi ya wanafunzi kutoka chuo hicho kujifunza kwa vitengo huku akisema amefurahishwa na uwepo wa maabara nzuri inayoendesha huduma kwa ubora na kusema kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma itakua sehemu sahihi katika kutimiza adhima ya ushirikiano huo.
“Tumefurahi tumeona mazingira na maeneo mengine ya huduma yako vizuri kama maabara na idara mbalimbali hivyo tunatumaini kuwa wanafunzi wataweza kupata mazingira bora ya kujifunza kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kubadilisha ujuzi baina ya wataalamu wa hapa Hospitali na wataalamu kutoka katika chuo chetu” amesema Profesa. Ballandya.
Profesa. Enica Richard, ambaye ni Rais Ndaki ya Tiba amesema, katika ushirikiano huo zipo faida nyingi ambazo zitapatikana kwa pande zote mbili kubwa likiwa ni kubadilishana ujuzi , kujengewa uwezo kwa wataalamu wa hospitali lakini pia ongezeko la wataalamu katika utoaji wa huduma kutokana na uwepo wa wanafunzi wa kada mbalimbali katika eneo hilo.
“Kwanza ninapenda kuwapongeza, nipende kusema kuwa kwa hiki tulichokiona hususani maabara na sehemu nyingine basi nieneo sahihi sana katika kujenga ushirikiano imara baina yetu, pia hii itawapa wigo mpana wanafunzi na wataalamu katika taasisi zote mbili kuweza kubadilishana ujuzi” amesema Profesa. Enica Richard.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma Dkt. Lameck Mdengo ameushukuru uongozi wa Chuo cha (MUHAS) kwa kuchukua hatua ya kujenga ushirikiano imara na Hospitali na kubainisha kuwa ushirikiano huo unaleta tija katika uboreshaji wa huduma na utoaji wa huduma kwa wananchi kupia mafunzo na kujengeana ujuzi baina ya wataalamu.
“Mimi niseme tu kuwa napenda kuwashukuru sana kwa ujio huu, kama Hospitali tunaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuweza kufikia lengo la ushirikiano huu” amesema Dkt Mdengo, Mganaga Mfawidhi wa Hospitali.



